Wachina waja kuipanga Dar


Na Julius Mathias, Mwananchi
Dar es Salaam ni moja ya majiji yanayokua kwa kasi barani Afrika kutokana na kasi ya ujenzi wa majengo ya kisasa, kupanuka na kuongezeka kwa idadi ya watu.
Kukua huko kumeandamana na
adha nyingi zikiwamo za barabara zisizokidhi wingi wa magari, hivyo kusababisha foleni hata kukosa nafasi za maegesho, hasa maeneo ya katikati ya mji.
Hali hiyo inasababisha wakazi wake kupoteza muda mrefu wakiwa safarini kwenda kazini, kurejea nyumbani au kufanikisha shughuli zao za kiuchumi huku wengi wao wakiishi maeneo ambayo hayajapimwa.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Malazi mwaka 2012, Mkoa wa Dar es Salaam una wakazi 4,364,541, wanaume wakiwa 2,125,786 na wanawake 2,238,755 huku likiwa na asilimia 5.6 ya ongezeko la watu unaolifanya kuwa na wastani wa watu 4.0 kwa kila kaya.
Sensa hiyo inaonyesha kuwa msongamano wa watu ni mkubwa zaidi kwa Mkoa wa Dar es Salaam ukifikia watu 3,133 kwa kilomita moja ya mraba.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema kati ya mwaka 2004 na 2007, jumla ya miliki holela 274,039 zilitambuliwa katika Jiji la Dar es Salaam, huku nyingine 44,039 zikiandaliwa mpango wa urasimishaji maeneo ya Kimara na Mbezi ambako wananchi wamehamasishwa kuchangia gharama za upimaji.
Hata hivyo, kutokuwapo kwa udhibiti wa ujenzi, kumesababisha ufinyu wa barabara na ugumu wa kusambaza huduma kama vile maji.
Hata inapolazimu kuweka miundombinu kama ya barabara, inabidi fedha nyingi zitumike kwa sababu ya gharama kubwa za ulipaji fidia.
Ujenzi holela pia umesababisha njia za asili za maji kuzibwa na nyumba za makazi zilizojengwa. Matokeo yake, baadhi ya maeneo, mvua zinaponyesha maji yanakosa njia ya kutokea.
Hiki kimekuwa chanzo kikubwa cha mafuriko, hata maeneo kuwa hayapitiki. Kutokana na mazingira hayo, mvua kidogo zimekuwa zilisababisha athari kama za masika au vuli hivyo na kuwakwaza wakazi wengi.
Wakazi wa manispaa tatu za Jiji la Dar es Salaam wamekuwa wakijiuliza,tatizo hili linatokana na nini? Wengi wamekuwa na tafsiri nyingi tofauti.
Hata hivyo, hali halisi inaonyesha kwamba miundombinu ya jiji hilo imekuwa ikitengenezwa pasipo mipango yenye ubunifu wa kitaalamu tangu mwaka 1979.
Serikali inasemaje?
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata anakiri kutokuwapo kwa mipango miji ya jiji.
Anasema Serikali ilichelewa kugundua tatizo hilo, lakini iko mbioni kukabiliana nalo.
“Taratibu za kupata ‘master plan’ (mpango mji) zilianza tangu mwaka 2008 na sasa tayari tunayo rasimu itakayokamilishwa na picha za anga pamoja na zile za satalaiti.
“Tupo katika hatua za mwisho za kutoa zabuni ya picha hizo na mpaka kufikia Juni mwakani, tutakuwa tumekamilisha,” anasema Kidata.
Anasema Rais Jakaya Kikwete alizungumza na Serikali ya China ili isaidie kuipatia Tanzania wataalamu wa mipango miji.
Anasema wataalamu hao kutoka China kwanza watapewa kazi ya kuipanga miji ya Lindi, Mtwara, Kigoma na Kigamboni.
Baada ya kazi hiyo, watashughulikia Jiji la Dar es Salaam na kwamba kazi hiyo tayari imetengewa bajeti.
Anasema ukosefu mpango huo wa mji, ndiyo chanzo cha foleni za magari, ufinyu wa barabara, kuongezeka kwa makazi holela, migogoro ya ardhi na magonjwa ya mlipuko.
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa anaelezea hali hiyo kuwa ni chanzo cha kukwama kwa huduma nyingi kuwafikia wananchi, kurundikana kwa uchafu na mlipuko ya magonjwa.

“Ni vyema suala hilo likafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo ili kuboresha mambo mengi. Kwa mfano, manispaa yangu ina takribani watu 2.2 milioni, lakini ni wakazi 20,000 pekee wanaofikiwa na huduma ya maji ya Dawasco,” anasema.
Mkurugenzi msaidizi wa katika idara ya picha za kutoka angani Wizara ya Ardhi, Dk James Mtamakaya anasema Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuwa na mita za mraba 4,000 na ili kulipiga picha za sataliti, zaidi ya Sh100 milioni zinahitajika, ikiwa ni gharama ya Sh26,000 kwa kila mita ya mraba.
Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo na Usimamizi wa Majanga cha Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Robert Kiunsi anasema ili kuepuka mafuriko katika maeneo ya makazi, zinahitajika mbinu za hali ya juu za kuhakikisha kunakuwa na mifumo ya kuondoa maji taka.
“Maendeleo ya makazi yanayokua kwa kasi, yanahitaji kuwekewa miundombinu sahihi ya mifumo ya maji,” anasema Profesa Kiunsi.
Anasema kwa kawaida maji ya mvua yanatakiwa yafyonzwe ardhini, lakini kwa kuwa maeneo mengi yamejengwa, suala hilo haliwezekani tena.
Endapo miundombinu mibovu na isiyolingana na mahitaji haitarekebishwa, Jiji la Dar es Salaam linaweza kuwa moja ya majiji yenye kero nyingi za usafiri, mafuriko na milipuko ya magonjwa yatokanayo na uchafu.
Mipango ya kuwaleta nchini wataalamu wa mipango miji kutoka China, inaweza kuwa ni njia mwafaka ya kumaliza tatizo hilo.
chanzo: mwananchi

No comments:

Post a Comment